Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fatma Karume kusimamia kesi ya kumshtaki Rais, AG

31578 Pic+fatma Fatma Karume, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS)

Fri, 14 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai hana sifa na kwamba uteuzi wake umekiuka Katiba ya nchi.

Hivyo, Shaibu amemwelekeza mwanasheria wake, Fatma Karume kufungua kesi Mahakama Kuu ya Dar es Salaam dhidi ya Rais John Magufuli ambaye alimteua pamoja na Dk Kilangi aliyeteuliwa Februari.

Akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam, Shaibu alisema uteuzi wa mwanasheria mkuu haukufuata matakwa ya Katiba na kwamba Dk Kilangi hana sifa kushika nafasi hiyo.

Alisema Ibara ya 59 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetaja sifa ya mtu kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu ambayo ni kwanza, atateuliwa kutoka miongoni mwa watumishi wa umma; pili, mwenye sifa ya kufanya kazi kama wakili na tatu, awe amekuwa na sifa hizo kwa muda wa miaka 15 au zaidi.

“Dk Kilangi hana sifa hizo zote, anaweza ku-resign kwa heshima yake, unawezaje kukaa hapo wakati unajua huna sifa, go back to teach (urudi kufundisha). Anaweza kuwa mwanasheria mzuri lakini kwa nafasi ile hana sifa,” alisema Shaibu.

Alisema amemhusisha Rais Magufuli katika kesi hiyo kwa sababu yeye ndiye aliyefanya uteuzi huo aliodai kuwa unakiuka Katiba..

Alisema utafiti alioufanya, amebaini Dk Kilangi alisajiliwa kuwa wakili mwaka 2011, hivyo amefikisha miaka saba kama wakili badala ya miaka 15 inayotakiwa Kikatiba.

Pia, alisema amebaini tangu 2004, amekuwa akifanya kazi kwenye taasisi mbalimbali binafsi wakati Katiba imebainisha kuwa lazima mwanasheria mkuu awe mtumishi wa umma ambaye amefanya kazi kwa zaidi ya miaka 15.

Alidai kuwa kati ya mwaka 2001-2004, Dk Kilangi alikuwa akifanya kazi katika ubalozi wa Denmark nchini; mwaka 2005-2008 alikuwa mhadhiri wa muda Chuo Kikuu cha Ruaha na Tumaini.

Mwaka 2008, aliajiriwa na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino kama mshauri wa wanafunzi na mhadhiri, nafasi ambayo aliitumikia kabla ya kwenda Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura) mwaka 2017.

Wakili Fatma Karume alikiri kupokea maelekezo ya Shaibu na alisema aliandikisha shauri hilo jana.

Hata hivyo, akizungumzia suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju alisema hawezi kutoa ufafanuzi kuhusu yanayoitwa malalamiko ya Shaibu kwa sababu hajui amesema nini na amelalamika kuhusu sheria ipi iliyokiukwa.

“Tukiona au kumsikia msingi wa malalamiko yake, tutatoa taarifa rasmi ya Serikali,” alisema Mpanju.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Fatma Karume ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alikiri kupokea maelekezo hayo kutoka kwa Shaibu na jana alisema alikwenda kuandikisha shauri hilo.

“Ni kweli nimepokea maelekezo Msajili hayupo, kwa hiyo tunasubiri akirudi aisajili kesi ili ianze kusikilizwa,” alisema Fatma.

Mwanasheria huyo alisema Rais Magufuli ameunganishwa kwenye kesi hiyo kwa sababu ndiye aliyemteua na uteuzi huo umevunja Katiba ya nchi. Alisema Mahakama ndiyo itatoa mwongozo wa shauri hilo.



Chanzo: mwananchi.co.tz