Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fatma Karume akwaa kizingiti kingine

39903 Pic+fatma Fatma Karume

Tue, 13 Jul 2021 Chanzo: ippmedia.com

​​​​​​​JAMHURI imewasilisha nia ya kukata rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotengua uamuzi wa kumfuta katika orodha ya mawakili, Fatma Karume.

Nia hiyo ya kukata rufani imekwamisha maombi ya Fatma kupitia Wakili wake, Peter Kibatala, ya kutaka Msajili wa Mahakama Kuu atoe amri na kuelekeza mteja wake aendelee kufanya kazi ya uwakili.

Wakili Kibatala aliandika barua kwa Msajili wa Mahakama Kuu, akiomba mteja wao Karume aendelee kufanya kazi ya uwakili kama Mahakama hiyo ilivyoamuru Juni 21, mwaka huu.

Katika barua hiyo aliomba Msajili wa Mahakama Kuu aamuru na kuelekeza kwamba leseni namba 848 ya Karume iliyozuiliwa iendelee kutumika kwa kazi ya uwakili.

Msajili Sharmilla Sarwatt katika majibu yake aliwafahamisha kwamba mlalamikiwa Jamhuri katika rufani namba 2/2020 iliyokuwa Mahakama Kuu aliwasilisha nia ya kukata rufani akipinga uamuzi wa Mahakama hiyo uliotolewa Juni 21, mwaka huu.

Mahakama Kuu Masjala Kuu ilitengua uamuzi wa Kamati ya Mawakili iliyomfuta Karume katika orodha ya mawakili nchini.

Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, likiongozwa na Jaji Issa Maige, Jaji Deo John Nangela na Jaji Edwin Kakolaki.

Jopo hilo lilitoa uamuzi huo kutokana na rufani iliyokatwa na Karume akipinga uamuzi wa kusimamishwa uwakili uliotolewa na Kamati ya Mawakili.

Karume alifutiwa uwakili na kamati hiyo Septemba 23, mwaka 2020 kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Adelardus Kilangi, akimtuhumu kukiuka maadili ya taaluma kwa kutumia lugha ya kumdhalilisha wakati akiwasili hoja za maandishi katika shauri alilokuwa akimwakilisha mteja wake Ado Shaibu.

Jaji Kiongozi, Dk. Eliezer Feleshi, alimsimamisha uwakili kwa muda Karume kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa na mawakili wa serikali katika kesi waliyokuwa wakimwakilisha Profesa Kilangi na Dk. John Magufuli na kuelekeza malalamiko hayo yasikilizwe na kamati.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake wa kutengua ilikubaliana na sababu moja pekee ya rufani hiyo ambayo ilitosha kutengua uamuzi wa kamati hiyo.

Katika sababu hiyo ambayo Mahakama Kuu ilikubaliana nayo, Karume kupitia kwa wakili wake alidai kuwa kamati haikuwa na mamlaka ya kusikiliza malalamiko ya Profesa Kilangi kwa kuwa ilikuwa inakiuka uamuzi wa Jaji Kiongozi.

Mawakili wanaomtetea Fatma, Peter Kibatala na Dk. Rugemeleza Nshalla walipinga uamuzi wa kumsimamisha uwakili mteja wao uliotolewa na Kamati ya Maadili baada ya Jaji Kiongozi, Eliezer Feleshi mwaka 2019 kuelekeza shauri hilo likasikilizwe na kamati hiyo na kabla ya kufanya hivyo kamati ilianza kusikiliza malalamiko ya Kilangi.

Jopo hilo baada ya kupitia hoja mbalimbali zilizowasilishwa lilitengua adhabu ya kufutiwa uwakili na kutoa amri kwa ajili ya utekelezaji.

Mahakama katika uamuzi wake iliamuru malalamiko yapelekwe katika Kamati ya Mawakili watakaotoa uamuzi dhidi ya Karume.

"Kwa uamuzi huo Fatma atakuwa na nafasi ya kujitetea, amerudishiwa uwakili wake, hivyo anayo haki ya kujitetea," alisema Dk. Rugemeleza Nshalla.

Pia Mahakama Kuu iliamuru Msajili wa Mahakama hiyo ndio apeleke malalamiko kwenye kamati ya mawakili.

Mahakama Kuu ilifuta mwenendo wote wa kamati ya maadili ya mawakili na kwamba hoja zao za kupinga kufutiwa uwakili Karume zilikuwa 13.

Karume alisimamishwa kazi huku sababu yake ikitajwa kuwa kile alichokizungumza katika kesi iliyofunguliwa na Ado.

Mawakili wa serikali walilalamikia maneno yalioandikwa na Karume wakati walipokua wakifungua kesi hiyo Mahakama Kuu.

Anadaiwa kuandika "hata iwapo kesi hii itashindwa, ataendelea kupambana nayo, rais akiondoka madarakani mwaka 2020 au kama ataondoka 2025 au kama mahakama itabadilika ataendelea kupambana”.

Chanzo: ippmedia.com