Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fatma Karume akemea tabia ya kuwakamata mawakili

50865 Pic+mawakili

Sun, 7 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kimesema tabia iliyojengeka ya kuwakamata mawakili wakati wakitimiza majukumu ya kuwatetea watuhumiwa walioko mahabusu ni kuminya uhuru na mahakama na utawala wa sheria.

Rais wa TLS anayemaliza muda wake, Fatma Karume amesema hayo leo Ijumaa Aprili 5, 2019 katika mkutano wa mwaka ambao utaambatana na kuwachagua viongozi wapya kesho Jumamosi watakaokiongoza chama hicho katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.

Amesema licha ya changamoto hiyo wamejiwekea utaratibu wa kuendesha programu za mafunzo kwa wanachama vijana ili kuwa na chama imara chenye kujiongoza bila kuingiliwa na mamlaka nyingine.

“Ni muhimu tukaweza kujisimamia mambo yetu wenyewe bila kuingiliwa na hili litafanikiwa iwapo tumekuwa na utaratibu wa kurithisha misingi ya uongozi kwa wanasheria wapya ili kuendeleza utawala bora kwenye chama chetu ambacho kinahitajika sana katika kuhimiza utawala wa sheria,” amesema.

Amesema bila uhuru kwa wanasheria katika kutekeleza majukumu yao kuna uwezekano ikafika siku watuhumiwa wa kesi mbalimbali wakanyimwa haki ya kutetewa kwenye vyombo vya kisheria au mawakili kunyang’anywa leseni za uwakili.

Fatma amesema ni wajibu wa kila mwanasheria kupigania uhuru wa kufanya kazi bila kubughudhiwa kinyume cha sheria kwani kuona ni sawa wanapofanyiwa uonevu na wenye mamlaka ni kukiuka utawala unaozingatia sheria.

Ameongeza yapo matukio ambayo mawakili wamekwenda vituo vya polisi kuwatetea wateja wao badala yake maagizo ya viongozi wa serikali yalitoka kwa kuagiza mawakili wawekwe mahabusu bila kuvunja sheria yoyote jambo lisilokubalika.

“Uhuru wa wanasheria katika kutekeleza wajibu wao unalindwa na mikataba ya kimataifa ambayo nchi yetu ni mwanachama na inapaswa kulinda haki hiyo ili ustawi wa kila mmoja uendelee kulindwa katika misingi ya kisheria,” amesema Karume.

Naye Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samata amewataka wanasheria na viongozi katika nafasi mbalimbali nchini kuheshimu na kufuata utawala wa sheria kwani sheria ndio msingi wa maendeleo ya nchi yoyote duniani na ndio msingi wa haki.

Amewataka wanasheria kujiendeleza kwa kusoma vitabu mbalimbali na kufananisha vitabu kama rafiki wa kweli katika maisha wasomi ambao wanataka kuendelea na kujifunza kutoka wasomi waliotangulia kwa mafanikio.

“Nyumbani kwako ukiwa na vitabu 50 hii ina maana una marafiki wa ukweli ndani kwako 50, humo ndani wapo wanasheria, majaji na wengine ambao hautajuta kuwa nao kwa sababu kila mara watakuongezea maarifa mapya.” amesema Jaji Samata.

Awali, katika semina ya wanasheria wenye ulemavu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Amon Mpanju amesema mawakili wenye ulemavu wanashindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo kama mawakili wasio na ulemavu.

Ameitaka TLS kuwawezesha mawakili wenye ulemavu kwa sababu wanahitaji vifaa maalumu ambavyo vitawawezesha kuwa na ofisi zao za uwakili ambazo gharama zake ni kubwa zaidi lakini ni muhimu ili kujitegemea.

“Kuwa na ulemavu si kubaki ombaomba bali yaangaliwe mazingira wezeshi ya kumwezesha kutekeleza wajibu wake wa kitaaluma licha ya changamoto za kuwachukulia watu wenye ulemavu kama watu wasio na msaada wowote katika jamii,” amesema Mpanju.



Chanzo: mwananchi.co.tz