Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fatma Karume: Uchaguzi TLS hauna mizengwe

50061 Fatmapic

Wed, 3 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume amesema anaamini mrithi wake atakayechaguliwa Aprili 6, 2019 atapatikana katika mazingira ya haki kwa vile ni utaratibu wa chama hicho kupata viongozi wake bila mizengwe.

Chama hicho kilichoasisiwa mwaka 1954 kwa sheria ya Bunge kitafanya uchaguzi wake wa kila mwaka jijini Arusha na ripoti zinasema baadhi ya wajumbe wameanza kuwasili jijini humo wakishiriki semina kuelekea kwenye uchaguzi wenyewe.

Akijibu swali la Mwananchi kuhusu mwelekeo wa uchaguzi huo, rais huyo ambaye hagombei tena amesema leo Jumanne Aprili 2, 2019 kwamba hana shaka wanasheria wataendeleza desturi yao ya kupata viongozi bila mizengwe.

Amesema kamati ya uteuzi haitegemei kumwonea mgombea yeyote na kusisitiza inafanya kazi yake kwa uhuru na haki.

“Hatujawahi kuwa na uchaguzi usiokuwa huru na haki na suala hilo halijaanza leo wala jana,” amesema wakili huyo wakati akizungumza kwenye ofisi za chama hicho zilizoko Mtaa wa Regent jijini Dar es Salaam.

Amesema kwa vile ni sehemu ya utamaduni wa chama hicho kufanya chaguzi zake kwa kuzingatia haki na uhuru, hali hiyo inatarajiwa kushuhudiwa pia wakati wanasheria hao watakapokutana mwishoni mwa wiki kumchagua mrithi wake.

“Na yule atakayechaguliwa na wanachama ndiye atapata urais wa Tanganyika Law Society na atatuendesha kwa mwaka mmoja,” amesema rais huyo ambaye alichaguliwa kwenye nafasi hiyo mwaka 2018 kuchukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Tundu Lissu.

Fatma Karume anakuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa huo tangu chama hicho kilipoanza kufanya kazi mwaka 1954.

Katika uongozi wake imeshuhudiwa chama hicho kikiwa mkosoaji mkubwa wa baadhi ya sheria zinazodaiwa kukandamiza uhuru wa maoni ikiwamo sheria mpya ya vyama vya siasa iliyoanza kufanya kazi hivi karibuni.



Chanzo: mwananchi.co.tz