Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fatma Karume, Serikali ni mnyukano mkali

Fatma Karume Uwakili Fatma Karume

Sat, 23 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mvutano wa haki ya wakili wa kujitegemea, Fatma Karume kufanya shughuli za uwakili Tanzania Bara unazidi kuchukua sura mpya, baada ya Mahakama ya Rufani kukubali kusikiliza shauri la maombi ya Serikali ya ruhusa ya kukata rufaa kupinga mwanasheria huyo kurejeshewa haki hiyo.

Mahakama hiyo imekubali kusikiliza shauri hilo baada ya kukataa ombi la wakili Karume kupitia kwa wakili wake, Peter Kibatala, kufuatia pingamizi lake licha ya kukubaliana na hoja za pingamizi hilo kuhusu kuwepo kwa kasoro za kisheria katika shauri hilo la Serikali.

Serikali ilifungua shauri la maombi mahakamani hapo ikiomba ruhusa kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, iliyomrejeshea uwakili Fatma aliofutiwa na Kamati ya Mawakili iliyomtia hatiani kwa kosa la ukiukwaji maadili ya kitaaluma.

Awali, Serikali ilifungua maombi hayo ya ruhusa Mahakama Kuu ambayo iliyakataa, ndipo ikaenda kuomba ruhusa hiyo Mahakama ya Rufani, lakini wakili wake, Kibatala aliibua pingamizi la awali akiiomba Mahakama hiyo isilisikilize shauri hilo bali ilitupilie mbali.

Katika pingamizi hilo alidai shauri hilo halina ustahilifu kwa kuwa kiapo kinachounga mkono hati ya maombi hakijaambatanishwa na amri ya Mahakama Kuu inayopingwa ya kuinyima ruhusa kwa mujibu wa kanuni ya 49(3) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo Wakili wa Serikali, Erigh Rumisha licha ya kukiri kasoro hiyo, aliiomba mahakama kutumia kanuni ya kupuuza ukiukwaji wa matakwa ya kisheria usioathiri kesi ya msingi, na kuendelea na usikilizwaji shauri la msingi.

Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa na jopo la majaji watatu, Jacobs Mwambegele (kiongozi wa jopo), Zephrine Galeba na Leila Mgonya imekubaliana na hoja za wakili Kibatala kuwa kutokana na ukiukwaji huo wa kikanuni shauri hili halina ustahilifu.

Hata hivyo, mahakama hiyo imesema baada ya kurejea kiapo cha wakili wa Serikali, George Mandepo katika aya ya 15 kimetaja kuwa hati ya maombi imeambatanishwa na amri ya Mahakama Kuu ya kukataa maombi yake ya kwanza ya ridhaa ya kukata rufaa.

Kwa sababu hizo, mahakama hiyo imesema kutokuambatanishwa kwa amri hiyo ya mahakama ya kukataa maombi yake ya kwanza ya ridhaa kulikuwa ni kupitiwa bila kukusudiwa.

Hivyo imeamua hilo shauri linakidhi mahakama hiyo kwa mamlaka yake kutumia kanuni ya kutokuzingatia ukiukwaji matakwa ya kisheria na hivyo kuendelea kusikiliza shauri la msingi badala ya kulitupilia mbali.

Mahakama hiyo imesema inatambua mgogoro katika shauri hilo unahusu haki ya mwanasheria huyo kufanya kazi ambayo imesimamishwa kwa zaidi ya miaka minne sasa, na kwamba huo ni muda mrefu kwa mtu anayepigania haki hiyo kama anastahili kufanya kazi au la.

Hata hivyo, ilisema katika picha pana inaonyesha kwamba kulitupilia mbali shauri hilo katika hatua hiyo, hata kama ilipaswa kufanya hivyo hakutakuwa na unafuu kwa upande wa mwanasheria huyo, kwa kuwa uamuzi huo kisheria hautamaliza mgogoro.

Kwa mamlaka yake chini ya Sheria ya Mamlaka ya Rufaa Kanuni za Mahakama ya Rufani imeipa Serikali nafasi ya kukidhi matakwa ya kanuni ya 49(3) ya Kanuni (za Mahakama ya Rufani) ili shauri hilo liwe tayari kwa usikilizwaji.

Hivyo mahakama hiyo imeipa Serikali siku 30 tangu siku ya uamuzi huu ulipotolewa Septemba 11 mwaka huu, kuwasilisha kiapo cha nyongeza kikiwa kimeambatanishwa na amri ya Mahakama Kuu, ikikataa maombi ya ruhusa ya kukata rufaa kukidhi.

Iliahirisha usikilizwaji wa shauri hilo mpaka kikao cha mahakama kijacho kwa tarehe ambayo itapangwa na msajili wa Mahakama. Mwanzo wa mgogoro

Mgogoro wa uwakili wa mtoto huyo wa Rais wa awamu ya Sita wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Aman Abeid Karume na pia rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ulianzia katika mwenendo wa kesi ya Kikatiba namba 29 ya mwaka 2018.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu akipinga kuteuliwa kwa Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akidai hakuwa na sifa, lakini Serikali ilimwekea pingamizi la awali.

Akijibu hoja za pingamizi hilo, pamoja na mambo mengine Fatma alidai Profesa Kilangi bado ni mchanga kitaaluma, hana uwezo wa kusimamia jukumu la uwanasheria Mkuu wa Serikali na amekuwa akiipotosha Serikali katika mambo mengi.

Kutokana na kauli hizo, Wakili Mkuu wa Serikali (SG) aliwasilisha malalamiko, kwamba kauli hizo ni kinyume na kanuni za maadili ya mawakili, ni kejeli na kashfa ya kudhalilisha ofisi ya AG.

Kufuatia malalamiko hayo, Septemba 20, 2019 Jaji Kiongozi Dk Eliezer Feleshi alimsimamisha Fatma Karume kwa muda kutoa huduma za uwakili chini ya kifungu cha 22(2) (b) cha Sheria ya Mawakili, kusubiri malalamiko dhidi yake kuwasilishwa na kuamuriwa na Kamati ya Mawakili.

Pia, alimwelekeza msajili wa Mahakama Kuu kuwasilisha malalamiko hayo kwenye kamati hiyo.

Fatma alifungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani akiiomba mahakama hiyo itengue uamuzi huo wa Mahakama Kuu wa kusimamishwa kwake. Baadaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali alimfungulia Fatma mashtaka katika Kamati ya Mawakili, kupitia shauri namba 29 la mwaka 2019, akiiomba kamati hiyo imuondoe katika orodha ya mawakili kwa madai ya ukiukaji maadili ya mawakili kutokana na kauli hizo.

Kamati hiyo katika uamuzi wake Septemba 23, 2020 ilimfuta Fatma Karume katika orodha ya mawakili baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukiuka maadili ya taaluma hiyo, lakini alikata rufaa Mahakama Kuu Masjala Kuu akipinga uamuzi huo wa Kamati ya Mawakili.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu, Issa Maige (kiongozi wa kopo), Dk Deo Nangela na Edwin Kakolaki Juni 21, 2021, ilibatilisha uamuzi wa Kamati ya Mawakili, kufuatia hoja ya pingamizi la Fatma.

Ilisema kuwa kwa kuzingatia uamuzi wa mahakama, wa jaji Feleshi, AG hakuwa na haki ya kupeleka malalamiko hayo kwa kamati hiyo, isipokuwa msajili, na kwamba kamati hiyo kusikiliza na kuamua shauri hilo ilikuwa inakwenda kinyume na amri ya Jaji Kiongozi.

Serikali haikuridhishwa na hukumu hiyo, hivyo iliomba kibali Mahakama Kuu, ili ikate rufaa, kuipinga.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Stephen Magoiga Desemba 17, 2021, iliinyima Serikali kibali cha kukata rufaa kwa kushindwa kuthibitisha kuwepo kesi au hoja zinazopaswa kuamuriwa na Mahakama ya Rufani, ndipo ikafungua maombi haya.

Lakini Juni 27, 2023, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake uliotolewa na jopo la majaji watatu, Augustine Mwarija (Kiongozi wa jopo), Dk Paul Kihwelo na Mwanaisha Kwariko, ilitupilia mbali shauri la mapitio la Fatma.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo kufuatia pingamizi la awali la Serikali kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu kumsimamisha Fatma uwakili haukupaswa kupingwa Mahakama ya Rufani kwa njia ya mapitio.

Mahakama hiyo ilisema kuwa kifungu cha 22(2) (b) cha Sheria ya Mawakili, ambacho Mahakama Kuu ilikitumia kumsimamisha Fatma, pia kinaipa mahakama hiyohiyo mamlaka ya kuondoa amri hiyo, hivyo Fatma alipaswa kufungua maombi Mahakama Kuu kuomba kuondolewa amri hiyo ya kusimamishwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live