Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chungu na tamu za Mfugale flyover

20324 CHUNGU+PIC TanzaniaWeb

Tue, 2 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rais John Magufuli ameweka alama nyingine katika maisha ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam. Alama hiyo inachagizwa na uamuzi wa Aprili 16, 2016 baada ya kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya juu (flyover), iliyopo katika makutano ya Barabara za Nyerere na Mandela eneo laTazara.

Mkataba wa ujenzi wa flyover hiyo kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Kampuni ya Sumitomo Mitsui Construction Co. Ltd ulisainiwa Oktoba 15, mwaka 2015 chini ya Rais Magufuli wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi.

Kabla ya kuwapo kwa barabara hiyo ya juu, madereva wa magari binafsi na daladala wanasema walikuwa wakitumia wastani wa dakika 90 hadi 120 kusubiri upande mmoja wa magari kuruhusiwa kuvuka kwenye taa za makutano hayo hususan asubuhi na jioni.

Hata hivyo, mapinduzi makubwa yameonekana baada ya kuanza kutumika kwa flyover hiyo siku chache kabla ya uzinduzi rasmi uliofanyika Septemba 28, mwaka huu ukiongozwa na Rais Magufuli aliyeitambulisha flyover hiyo kuwa sasa itaitwa Mfugale Flyover.

Rais Magufuli anasema jina hilo linalenga kumuenzi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale kutokana na utumishi wake wa muda mrefu akihudumia eneo la uhandisi hususani wa barabara na kufanikiwa kufanya mambo makubwa yaliyofanikisha ujenzi wa madaraja mbalimbali yanayotegemewa katika kuifungua na kuiunganisha mikoa ya Tanzania na hata nchi za jirani.

Kwa mujibu wa Tanroads, kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda wa kukaa kwenye foleni kwa asilimia 80, ikimaanisha kutoka dakika 45 hadi 10 za kuvuka kwenye makutano hayo.

Dereva Wansislaus Shoo anasema kabla ya kufunguliwa kwa barabara hiyo, alikuwa akitumia wastani wa saa mbili kutoka kwenye foleni ya eneo hilo la makutano hatua iliyoathiri shughuli zake za kibiashara.

Naye kondakta wa daladala linalofanya safari zake kati ya Vingunguti na Temeke, maarufu kwa jina la Said, anasema kukamilika kwa daraja hilo kutasaidia kuongeza idadi ya ruti (safari) anazofanya kwa kila siku, hivyo kuongeza kipato.

“Foleni ya Tazara ilituumiza sana sisi watu wa biashara ya usafiri, ilinifanya nizunguke ruti nne hadi tano tu kwa siku, lakini kwa dakika zitakazopungua kutokana na ujenzi wa flyover, itanisaidia kuzunguka ruti sita hadi saba. Kiukweli nashukuru sana kwa ujenzi wa barabara hii,” anasema kondakta huyo.

‘Maumivu’ ya Flyover

Kutokana na mazingira ya foleni, wafanyabiashara walikuwa wakitumia fursa hiyo kufanya biashara kwa abiria wa magari yaliyokuwa yakikaa muda mrefu kwenye foleni. Waendeshaji wa bodaboda nao walitumia fursa ya foleni kupakia abiria wenye haraka ya kuwahi ofisini, nyumbani au kwenye shughuli mbalimbali.

“Wengi wamehama hapa kwa kuwa sasa hakuna biashara tena. Daladala hazikai sana kwenye foleni na nyingi zinapita kwenye flyover. Awali kwa siku nilikuwa nikipata kati ya Sh30,000 hadi Sh40,000, lakini sasa kuipata Sh20,000 ni mbinde, bodaboda wengi wamehamia foleni za Buguruni,” anasema Andrew Petro anayefanya biashara za mkononi katika eneo la Tazara.

Wauzaji wa bidhaa za chocolate, maziwa na biskuti, pia walisema barabara hiyo imewafanya wengi wao kuondoka eneo hilo.

“Ilikuwa ni kawaida sana kuuza Sh70,000 au Sh80,000 katika eneo hili la foleni ya Tazara, lakini sasa baada ya kuondoka imekuwa vigumu hata kupata Sh50,000. Wastani wa baiskeli 40 kati ya 50 zilitegemea eneo hili,” anasema Frank James, mmoja wa wachuuzi hao.

Mfanyabiashara wa mihogo na karanga mbichi katika makutano hayo, Neema Chaula anasema kabla ya uwepo wa barabara hiyo, alikuwa akiingiza hadi Sh4,500 kwa siku, lakini kwa sasa amekuwa akiuza wastani wa Sh1,500 tu kutokana na kupungua kwa foleni.

Madereva wa bodaboda ni miongoni mwa kundi la waathirika waliotumia fursa ya foleni kupakia abiria wenye haraka ya kuwahi kazini na kwenye shughuli mbalimbali.

“Kwa siku nilipata Sh30,000 hadi Sh40,000 lakini sasa kuipata Sh20,000 ni shida. Daladala hazikai sana kwenye foleni na nyingi zinapita kwenye flyover, matokeo yake bodaboda wengi wamehamia foleni za Buguruni,” anasema Andrew Petro ambaye ni miongoni mwa bodaboda ambao walikuwa wakitumia fursa ya foleni katika makutano hayo.

Maumivu mengine yameonekana kwa abiria wanaotegemea daladala zinazofanya safari kati ya Mnazi Mmoja na Gongo la Mboto ambazo sasa zinapitiliza kwa kutumia barabara ya juu, hivyo kuwafanya wale wanaosubiri usafiri katika vituo vya Tazara kusota kwa muda mrefu na wakati mwingine kuukosa, hivyo kuwalazimu kusogea kwenye vituo vya mbele.

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Johansen Kahatano anasema tayari changamoto hiyo wameshaibaini na inashughulikiwa kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara (Tanroads).

Baadhi ya abiria waliozungumza na gazeti hili wanasema kwa sasa wanatumia zaidi ya dakika 10 hadi 60 kabla ya kupata daladala za Gongo la Mboto-Mnazi Mmoja zinazopitia barabara ya chini.

Tatizo hilo limeonekana zaidi wakati wa asubuhi na jioni pale daladala zinapokuwa zimejaza abiria kutoka vituo vikuu.

“Kabla ya kituo lazima niwaulize abiria kama kuna atakayeshuka, iwapo hakuna anayeshuka Tazara hakuna sababu ya kupita barabara ya chini. Inanirahisishia safari nipitapo juu moja kwa moja hadi kituo cha Mtava, na flyover inakuwa imenipunguzia muda wa kukaa foleni kwenye makutano,” anasema Said Mohamed, kondakta wa daladala za Gongolamboto-Mnazi Mmoja.

Uhai, ulinzi wa flyover

Wakati uchungu na utamu ukionekana, Serikali inaagiza ulinzi wa flyover hiyo itakayodumu kwa miaka 100 ijayo kuanzia mwaka huu. Barabara hiyo imejengwa kwa thamani ya Sh106.8 bilioni chini ya ufadhili wa Serikali ya Japan kwa kushirikiana na Tanzania.

Tanroads inamtaka dereva wa gari kutumia mwendo usiozidi kilomita 40 kwa saa anapopita kwenye flyover hiyo, kuzingatia sheria, utaratibu na kanuni za usalama barabarani wakati wote ikiwamo kutosimamisha gari katikati ya barabara hiyo ya juu.

Mhandisi Mfugale anasema barabara hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba tani 180 tu kwa wakati mmoja. “Haitakiwi kuzidi hapo na uhai wake ni miaka 100, ndipo itakapohitajika kujengwa upya.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameagiza kufungwa kamera za kurekodi matukio katika daraja hilo na kwamba wakandarasi waliojenga daraja kama hilo kuweka sehemu maalumu za kufungia vifaa hivyo kwa ajili ya usalama.

“Ili hata pale anapokuja mtu amelewa na kusababisha ajali tumjue ni nani hata kama atakimbia na gari lake. Tunatengeneza vitu vizuri ili vitusaidie sio kuleta matatizo,” anasema.

Miradi mingine Dar

Pamoja na mapinduzi ya flyover hiyo, Rais Magufuli anasema nchi imekuwa ikipoteza zaidi ya Sh400 bilioni kila mwaka kutokana na watu kutumia muda mwingi katika foleni, muda ambao wangeweza kuutumia katika uzalishaji mali.

“Kwa kulitambua hilo, tumeamua kuifanya Dar es Salam kuwa mpya, tutaboresha miundombinu ili kuondoa msongamano na kama Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam (Alhad Mussa Salum) alivyoomba flyover ziongezwe, nimhakikishie kwamba zipo nyingi zinakuja,” alisema Rais Magufuli wakati wa uzinduzi huo.

Rais Magufuli anasema iko miradi itakayoanza kutekelezwa siku chache zijazo na tayari serikali imeshatangaza tenda ya barabara kutoka Mbagala hadi Gerezani na Kivukoni-Chang’ombe hadi Magomeni umbali wa kilomita 21.

“Fedha hizi zitakazotumika ni mkopo wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), pia itajengwa flyover Chang’ombe na eneo la Mhasibu House au Machinjioni na tenda zimeshatangazwa,” anasema Rais Magufuli.

Mbali na Mfugale Flyover, nyingine zitakazojengwa ni ‘interchange’ (barabara za mwingiliano) iliyoanza kujengwa katika eneo la Ubungo kwa gharama ya Sh247 bilioni.

Magufuli anasema serikali imeamua barabara ya kutoka Kimara hadi Kibaha ijengwe njia sita kwa bajeti ya serikali na kugharimu Sh140 bilioni ili kuepusha msongamano.

Aidha, Rais Magufuli anasema kupitia mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) unajenga baadhi ya barabara na mfereji wa kilomita 40 wenye thamani ya Sh660 bilioni na kazi imeshaanza huku barabara zote zikijengwa kwa kiwango cha lami.

Mbali na hayo, pia aliagiza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Morocco hadi Mwenge yenye urefu wa kilomita 4.1 uanze kwa kuwa imechukua muda mrefu sasa tangu kutangazwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz