Busura Mabibi (70) mkazi wa Kijiji cha Kapalamsenga, Wilaya Tanganyika, Mkoa wa Katavi amefariki dunia baada ya kunyweshwa dawa na mganga wa kienyeji maarufu kama 'Kamchape', kwa kile kinachodaiwa alikuwa anajihusisha na vitendo vya ushirikina.
Akizungumzia tukio hilo, Emanuel Kalabwe ambaye ni mtoto wa marehemu ameeleza kuwa alipata taarifa ya kuwepo tukio la kutafuta wachawi nyumbani kwao, lakini hakuwa anatambua nani analeta waganga hao nyumbani na baada ya muda aliona kikundi cha watu kikiibuka na kumuomba mama yake atoke nje ili wafanye kazi yao.
Anasema licha ya kuhoji uhalali wa watu hao na kuomba vitambulisho ili kutambua wanakotoka na lengo lao, lakini mmoja wa watu walioambatana na wataalamu hao alimsikia akimtuhumu mama yake kuwa anajihusisha na uchawi.
"Yaani mama yangu amefariki kabla hata hajafikishwa kituo cha Afya Karema, alikuwa anatoa mapovu mdomoni na puani, naiomba sana serikali ichunguze kifo hiki na waliohusika washughulikiwe kisheria," amesema Kalambwe.
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amefika kijijini hapo kutoa pole na kusema kuwa tayari Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu wanaohusishwa na tukio hilo na kuahidi kuwa baada ya uchunguzi kukamilika watapandishwa mahakamani.
"Niwasihi ndugu wananchi tuwe watulivu serikali haijalala kwenye suala hili kwa kuanzia tayari watu hao watatu tunawashikilia katika vyombo vya ulinzi na usalama watatueleza kwa kina zaidi, tutachunguza kila kona kila uvungu na kila kitand,a ili kupata ukweli wa jambo hili," alisema Buswelu.