Waziri wa Kilimo, Husein Bashe amemtumia salamu Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina kuwa awe na shukrani kwa Serikali na kumtaka achezee Sekta nyingine sio kilimo ambayo ni tegemeo kwa Taifa.
Bashe amesema chokochoko za uongo za Mbunge Mpina zinapogusa Sekta ya Kilimo hawezi kumvumilia, kwa kuwa Taifa ni kubwa rasilimali ni chache hivyo jitihada zinazofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan haziwezi kurudishwa nyuma na yeye Bashe akakaa kimya ambapo amesema amejipanga kwenda Kisesa na kukutana na Wakulima ili kujua mbivu na mbichi na kusema yeye mwenyewe ni Mtoto wa uswahilini kama mbwai na iwe mbwai kwakuwa hataki utani na uongo katika Sekta hiyo inayogusa maisha ya Watu.
Waziri Bashe amesema hayo mara baada ya kuanza ziara ya kikazi katika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora ambapo ameanza kwa kukutana na Viongozi wa Bodi ya Pamba, Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wakulima wa Pamba na pia amezindua Mpango wa Kitaifa wa kuongeza tija katika uzalishaji wa pamba katika Kijiji cha Mbutu Wilayani humo.
“Watu hawalali usiku na mchana kutafuta suluhisho kwa Sekta hii, yeye alipewa nafasi akawa Waziri kwa zaidi ya miaka 20 alifanya nini, ni kweli haoni mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Serikali?, Serikali haiwezi kuwaletea Wakulima wanunuzi wezi, dawa feki na mbegu feki, Kisesa nakuja mtanijibu sitaki utani katika kilimo mshambulie Bashe sio hii Sekta hatuwezi kuwa na Taifa linatukana Watu linatukana Serikali tunakaa kimya, tunampa nafasi alete dawa, mbegu na kununua pamba, Nchi yetu tumekuwa na tamaduni ya kuacha Mtu anachafua Serikali na hana suluhisho, naenda Kisesa tutawauliza wakulima kama yale mawazo ni ya kwao Serikali tutaondoa huduma kama ni ya Mpina tutaacha….achezee Sekta nyingine sio kilimo Mimi nimezaliwa uswahilimi kama mbwai mbwai nimeamua”