Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso amemuondoa katika nafasi yake Meneja wa RUWASA wilayani Misungwi Mhandisi Marwa Kisibo kutokana na kutosimamia utekelezaji wa miradi ipasavyo katika wilaya yake. Waziri Aweso amefanya maamuzi hayo alipotembelea Mradi wa Maji wa Ukiliguru - Usagara - Kolomije - Sumve wa Chanzo cha Ziwa Victoria unaogharimu kiasi cha zaidi ya Bilioni 32 wilayani Misungwi na Kwimba Mkoa wa Mwanza.
Ziara hii ni Maelekezo ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Dkt Emmanuel Nchimbi alipofanya ziara yake mkoani Mwanza wilaya ya Simiyu na kupata malalamiko ya hali ya upatikanaji Maji na kusuasua kwa Miradi. Dkt Nchimbi alimuelekeza Aweso kufika Misungwi na kufanyia kazi changamoto zote.
Katika ziara hiyo, Mhe Aweso ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri. Mradi huu utanufaisha vijiji 19 wilaya ya Misungwi na vijiji 5 vya wilaya ya Kwimba vyenye jumla ya watu 85,400 na kuondoa kero ya maji katika maeneo makubwa ya Usagara na Nyashishi.
Aidha Aweso amezungumza na viongozi na wananchi wa Wilaya ya Misungwi na kutoa maelekezo mahususi ikiwa ni pamoja na Kuhakikisha mkandarasi wa mradi anafanya kazi usiku na mchana ili kazi hii ikamilike kwa wakati na kumuagiza Katibu Mkuu na Mtendaji mkuu wa RUWASA Wakae na mkandarasi anayejenga mradi huo Emirates Builders siku ya kesho tarehe 09/09/2024 pamoja na Wakandarasi wote wanaotekeleza Miradi ya Maji wilaya ya Misungwi.
Katika hatua nyingine Mhe Aweso ameelekeza mkandarasi anayejenga mradi wa Maji Illujamate - Buhingo aitwaye STC Costruction kwa gharama ya zaidi ya 12b pamoja na mkandarasi wa mradi wa maji Kigongo anayeitwa Mponela, miradi hiyo yote iliyopo wilayani Misungwi nao waitwe na Katibu Mkuu kujadili ukamilishaji wa miradi.