Morogoro. Wakati Spika wa bunge Ndugai akiagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu sakata la mwanamke kujifungua kituo cha polisi Mang’ula wilayani Kilombero, mwanamke huyo, Amina Mbunda , amesema bado anafuatwa na askari waliomkamata.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 12, Amina amesema askari Andrew Mapunda aliyemkamata siku ya kwanza alirudi jana Juni 11 na kumtaka asaini hati ya upekuzi.
Amesema akiwa nyumbani kwake majira ya mchana jana askari huyo alifika nyumbani na kumweleza kwa kuwa siku ya kwanza walifanya upekuzi bila kumsainisha karatasi yoyote, na kumuomba kufanya hivyo.
Amina amesema baada ya askari huyo kumweleza hayo alikataa na askari huyo aliondoka na kumwacha askari na mumewe wakizungumza.
Naye mume wa mzazi huyo,Abdallah Mrisho amesema ameshangazwa na askari huyo kuendelea kumfuata mkewe na kumtaka kusaini hati hiyo ya upekuzi.
“Kama ni makosa askari huyo alishalifanya tangu mwanzo pamoja na kushauriwa na yeye wakati walipompigia simu na kuwataka wasimchukue mkewe kutokana na hali yake,”amesema
Soma Zaidi: Spika Ndugai aagiza uchunguzi mwingine