Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alichojifunza Magufuli kwa Mengi

10557 Magufuli+pic TanzaniaWeb

Tue, 3 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameeleza namna alivyotafutwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi baada ya kupitishwa na CCM kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, huku akitaja vitu vikubwa vitatu alivyojifunza kutoka kwa mfanyabiashara huyo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai 2, 2018 katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Dk Mengi kiitwacho, ‘I can, I must, I will’, iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Kiongozi mkuu huyo wa nchi alikuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo.

Amesema baada ya kuteuliwa na CCM kugombea urais, Dk Mengi alimpigia simu na kutaka kuonana naye.

“Baada ya kuteuliwa na chama changu, Mzee Mengi alinipigia akaniambia anaomba kuniona, nikamwambia nipo mbali sana hataweza kuniona, (Mengi) akanijibu anataka kuniona na anajua kuwa nilikuwa nazunguka ila sikuwa na chochote, aliniambia kuwa anataka kunisaidia hata kuweka mafuta kuzunguka kufanya shughuli zangu,” amesema Rais Magufuli.

“Nikamwambia (Mengi) sitachukua huo mchango wako nisije kuanza kukusumbua kwa kuona namna gani nitaanza kulipa hizo fadhila. Nilimjibu kuwa nikirudi Dar es Salaam nitamuona.”

Amesema hata alivyorejea hakuweza kwenda kumuona, “lakini kikubwa ilikuwa ni kutaka kuwaonyesha kwamba ni mtu mwenye huruma, anajua watu wenye shida niliona sitaki nimkwaze mzee wa watu, pia nikawaza ukikusanya fedha kwa wafanyabishara kila mmoja utakuwa Rais wa namna gani wakati unataka wafanye biashara na wawe wakubwa zaidi.”

Rais Magufuli amesema Mengi ni mfanyabishara mzalendo na kupitia biashara zake mbalimbali ameleta maendeleo, ameshika nyadhifa mbalimbali na amewahi kushinda tuzo kadhaa ndani na nje ya nchi.

Akielezea mafanikio zaidi, amesema amejifunza mambo mengi kupitia mfanyabiashara huyo ikiwemo kutokukata tamaa.

“Watanzania tukiamua tunaweza, amezaliwa kwenye familia masikini sana lakini aliamua kukataa umasikini huo na hatimaye alifanikiwa,” amesema.

“Hii inatufundisha kuwa Watanzania wote tukiukataa umasikini wananchi wetu watapata maendeleo na nchi itaendelea. Watanzania tukijiamini tutaweza na tuache kukatishana tamaa.

Chanzo: mwananchi.co.tz