Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Agizo lingine kutoka kwa PM Majaliwa kuhusu "Tozo za Miamala"

571e95b6c6095713233c0bd1eeadd885 Miamala ya Simu

Tue, 3 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile waboreshe mapendekezo ya jinsi ya kuboresha mapato ya tozo za miamala ya simu.

Msemaji Mkuu wa Serikali, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Gerson Msigwa alisema jana Dar es Salaam kuwa, Majaliwa alitoa agizo hilo juzi baada ya viongozi hao kumkanidhi ripoti ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kufanyia kazi malalamiko ya wananchi kuhusu tozo hizo.

Msigwa alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa serikali katika kipindi cha robo ya mwisho ya mwaka wa fedha 2020/2021 kulichoishia Juni, mwaka huu.

Hivi karibuni Rais Samia aliagiza wizara hizo zifanyie kazi malalamiko ya wananchi kuhusu tozo kwenye miamala ya simu za mkononi katika kutuma na kupokea fedha.

“Mawaziri hao walikaa na wakaja na mapendekezo ya jinsi ya kupunguza malalamiko na waliwasilisha taarifa yao jana (juzi) kwa Waziri Mkuu ambaye naye aliwapa mawaziri hao maelekezo ya kuboresha taarifa hiyo,” alisema Msigwa.

Alisema serikali ilikuwa na kilio cha muda mrefu cha kuboresha huduma za jamii mfano maji, vituo vya afya, barabara na huduma nyingine nchini lakini ukosefu wa fedha ulikuwa kikwazo cha kufanikisha hayo na ndipo mawazo mbalimbali yalitolewa ya kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kutekeleza masukusanyo hayo.

“Tuna halmashauri zaidi ya 69 zinahitaji vituo vya afya nchini, hatuwezi kutimiza ujenzi wake kama hatuna fedha, sasa lengo la hiyo tozo ni kupata fedha kuboresha huduma hizo na serikali imekubali itapunguza kiasi cha tozo hiyo ila sio kuiondoa kwa kuwa hiyo ni utekelezaji wa sheria na kama ni kuondoa lazima irudi bungeni,” alisema Msigwa.

Alisema kilichofanywa ni Waziri Mkuu kutumia mamlaka aliyonayo kusheria kwenye kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo kuweka au kuagiza kuboreshwa au kupunguzwa kwa makato hayo lakini si kuiondoa.

Serikali iliweka tozo ya kati ya Sh 10 hadi Sh 10,000 kwenye miamala ya fedha kwa njia ya simu kulingana na kiasi kinachotumwa au kutolewa katika muamala husika. Awali, Msigwa alisema serikali inaendelea kukusanya mapato na kuendelea kutekeleza miradi yote ya maendeleo na ile ya kimkakati sambamba na kulipa watumishi wake mishahara na wazabuni mbalimbali.

Alisema kwa Julai, mwaka huu, serikali imetumia Sh bilioni 1.8 kuwalipa madiwani na wenyeviti wa halmashauri katika halmashauri ambazo hazipo kwenye kundi A la ukusanyaji mapato mengi.

Kuhusu hali ya uchumi, Msigwa alisema mfumuko wa bei bado uko chini wa asilimia 3.6 na kwamba uchumi utakuwa kwa asilimia 5.6 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Aidha, alisema serikali ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni dola za Marekani bilioni 5.5 ambazo zinatosha kufanya ununuzi wa bidhaa kwa kipindi cha miezi sita ijayo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz