Moshi. Kamera 16 za CCTV zimefungwa katika eneo la ujenzi wa kituo cha kimataifa cha mabasi cha Ngangamfumuni mjini Moshi ili kudhibiti wizi wa vifaa vya ujenzi.
Hayo yameelezwa na leo Alhamisi Agosti 29, 2019 na msimamizi wa mradi huo, Dickson Makweka wakati viongozi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Moshi Mjini walipofanya ukaguzi katika mradi huo.
Julai 18, 2019 waziri mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro, alitembelea mradi huo na kupokea taarifa ya wizi wa baadhi ya vifaa, zikiwemo nondo baada ya kutokea wizi wa tani tano za nondo.
Majaliwa aliagiza walinzi waliokuwa lindo siku wizi huo ukitokea kukamatwa.
"Kwa sasa hatutegemei kuona wizi ukitokea kwa kuwa tumefunga kamera za CCTV katika eneo hili, na hii inasaidia kudhibiti na kuimarisha usalama,” amesema Makweka.
Akitoa taarifa ya ujenzi huo, kaimu mhandisi wa manispaa hiyo, Edward Majengo amesema gharama za ujenzi huo utakaokamilika mwaka 2021 ni Sh28.8 bilioni, kwamba hadi sasa Serikali imeidhinisha Sh8.7 bilioni.
Pia Soma
- Wanafunzi wanaopata mimba shule ya Sekondari Kimagai wapungua
- 22 jela miezi sita kwa uzururaji, kujihusisha na biashara ya ngono
- Mikiki ya uchaguzi wa KKKT ilivyomrudisha Dk Shoo katika uongozi
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema juhudi za Serikali kutekeleza miradi zinaonekana na wataendelea kufuatilia kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wakati na mradi unakamilika kulingana na mkataba.
Ujenzi wa kituo hicho ulianza Januari 28, 2019.