Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amemuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aingilie kati ili Fatma Karume arejeshewe leseni yake ya uwakili aliyofutiwa Septemba 2019, baada ya kusimamia kesi aliyoifungua dhidi ya mtangulizi wake, Hayati John Magufuli.
Ado alitoa ombi hilo wakati akizungumza na MwanaHALISI Online hivi karibuni, kuhusu safari yake ya kisiasa, ambapo alisema kitu ambacho hatosahau maishani mwake ni uamuzi wake wa kumshtaki Rais Magufuli akiwa madarakani na katika kipindi ambacho watu wengi walikuwa wanamuogopa.
Kesi ambayo Ado alimfungulia Hayati Magufuli 2018 na kuwakilishwa na Fatma kabla ya kuvuliwa uwakili, ni ile ya kupinga uteuzi alioufanya wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Adelardus Kilangi, akidai ulikuwa batili kwa kuwa hakutimiza masharti ya katiba kushika nafasi hiyo.
“Katika kesi ile wakili wangu alivuliwa uanasheria kwa madai kuwa wakati wa kesi ile alitoa maneno makali na hata leo anapambana kupata kibali chake cha kuwa mwanasheria na natoa rai kwa Rais Samia, kuna mengi mazuri yamefanyika katika uongozi wake, kuhusu suala la Fatma Karume naomba ahakikishe anapata haki yake ili kutimiza dhamira yake ya kujenga maridhiano,” alisema Ado.
Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo
Akizungumzia hatma ya kesi hiyo aliyoifungua akiwa Katibu Mwenezi wa ACT-Wazalendo, Ado alisema hakufikisha lengo kwa kuwa aliangukia pua, lakini kitu pekee ambacho anajivunia ni uamuzi wake huo kufikisha ujumbe kwa umma ya kwamba Rais anaweza kushtakiwa akibainika amefanya uteuzi unaokiuka katiba.
“ilipokuwa mwenezi nilifanya maamuzi magumu sana niliamua kuchukua uamuzi wa kufungua kesi dhidi ya Rais jambo ambalo halikuwahi kufanywa katika kipindi chote cha miaka 30 ya vyama vingi. Haukuwa uamuzi mwepesi sababu niliieleza familia yangu kwamba nakwenda kuchukua uamuzi huu hakuna aliyenisikiliza wengi walidhani nimepatwa na kichaa katika kipindi ambacho watu wanapotea, wanafunguliwa kesi na kufungiwa biashara zao,” alisema Ado.
Mwanasiasa huyo kijana amesema anachojivunia katika uongozi wake wa kisiasa ni kuziibua changamoto za wananchi kisha serikali kuzitafutia ufumbuzi, hususan wakulima wa korosho, mbaazi na mazao mengine.
“Nilipokuwa katibu mwenezi kulikuwa na aina tofauti za kufanya siasa, wengine walifanya siasa za matukio na kushambulia watu ili kupata umaarufu lakini kwangu ilikuwa tofauti niliamua kufanya siasa za masuala na kuibua changamoto za watu ili niwe karibu na jamii, hadi ikafikia mahali wakawa wananiita msemaji wa mbaazi,” alisema Ado.