Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria wafurika treni ya SGR ikianza safari Dar- Dodoma

Sgr Treni (600 X 330) Abiria wafurika treni ya SGR ikianza safari Dar- Dodoma

Thu, 25 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza safari za treni ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, huku nauli ya chini ikiwa ni Sh31,000.

Treni hiyo imeanza safari hizo leo Alhamisi Julai 25, 2024, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Rais Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa mwaka jana, kwamba ifikapo Julai 2024 shirika hilo liwe limeanza safari hizo huku ikichukua saa tatu na dakika 25.

Treni hiyo iliyokuwa na mabehewa 14 na abiria zaidi ya 900, ilianza safari saa 12:00 asubuhi katika Stesheni Kuu ya Dar es Salaam.

Baadhi ya abiria waliozungumza na waandishi wa habari wamepongeza hatua hiyo wakisema itawarahisishia kuokoa muda na gharama.

"Kilichonisukuma kusafiri na treni hii ni mara yangu ya kwanza sijawahi kupanda treni, kwa hiyo ilikuwa ni kiu yangu kutumia usafiri huu.

“Nawashauri Watanzania wengine watumie usafiri wa treni kwa sababu ni bora na salama zaidi," amesema abiria aliyejitambulisha kwa jina la Joseph John.

Rose Mchau kutoka Mkuranga mkoani Pwani, amesema amefurahia kupanda treni hiyo kwa sababu ina mazingira mazuri na inatumia muda mchache.

Mkurugenzi Mtendaji wa TRC, Masanja Kadogosa amesema wanajivunia kutekeleza maagizo ya Rais Samia na kumshukuru kwa juhudi zake katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live