Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT-Wazalendo yamtaka Waziri Simbachawene kikao na msajili

ADO SHAIBU Katibu Mwenezi wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu

Thu, 9 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimesema kuwa katika kikao cha Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa, ni muhimu akawapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene.

Aidha, kimesema kama anataka kuwepo kwa suluhisho la mgogoro baina ya Polisi na Vyama vya Siasa kuhusu mikutano ya kisiasa ni lazima pande hizo ziwapo kwa kuwa polisi ni watekelezaji wa maagizo kutoka juu.

Akizungumza na Nipashe, Katibu Mwenezi wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu, alisema katika kufikisha ujumbe huo tayari, Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, amemwandikia msajili kumtaka waziri huyo awepo kwenye kikao hicho.

Kauli ya chama hicho, imekuja siku chache baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mtungi, kusema ataitisha kikao maalum cha wadau wa siasa kutafuta suluhu ya mivutano iliyojitokeza baina ya polisi na vyama vya siasa, hususan vyama vinapotaka kufanya makongamano au mikutano ya ndani.

“Jana (Juzi) Mwenyekiti Kabwe amemwandikia msajili kumtaka kuhakikisha waziri anakuwapo kwenye kikao hicho sababu polisi ni chombo kinachopokea amri tu kuzuia mikutano kutoka kwa viongozi hususan wakuu wa mikoa na wilaya, uwapo wake utasaidia kukumbushana ukweli maeneo ambayo sheria na kanuni mbalimbali hazifatwi na vipi zitekelezwe,” alisema Shaibu.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ina lenga kuleta mwanga juu ya hatima ya uhuru wa kikatiba juu ya makongamano na mikutano ya kisiasa nchini, kwa kuwa suala hili limepigiwa kelele hususan vyama vya upinzani kwa takribani miaka sita sasa.

Kwa mujibu wa Shaibu, ni mapema sana kuweka matumaini makubwa juu ya kikao hicho lakini chama chake kitashiriki na kupeleka mapendezo pamoja na kufikisha hoja husika, ili kuleta msukumo wa mageuzi ya uendeshaji wa siasa nchini kwani kukimbia meza ya mazungumzo siyo suluhisho.

Juzi, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema kauli ya Msajili kuhusu mikutano na makongamano inakiuka sheria na kanuni.

Aidha, siku hiyo hiyo Msajili Jaji Mutungi, alitoa taarifa kwa umma na kueleza chama hicho kimepotosha kauli yake kwa kuwa hajazuia mikutano wala makongamano, bali amevishauri vyama kwa kipindi vinapojaribu kupata ufumbuzi wa mvutano uliopo ni busara vyama kujizuia kufanyua shughuli zitakazosababisha kurudi kwenye hali hiyo.

Chanzo: ippmedia.com