Wakazi 12 wa Sumbawanga Mkoani Rukwa leo Juni 5, 2024 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia fedha kiasi cha Sh 9,200,000 kwa njia ya udanganyifu kwa kutuma jumbe zenye ushawishi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Pius Mahali(29), dereva bodaboda, Best Sinyangwe (24), mkulima, Andrea Kipeta (31), Dereva Lusekelo Jimmy (32), mkulima, Michael Kanyegele (28).
Wingine ni wakulima, Lucas Mpandezi(19), Steven Selemani (18), Emanuel Kawimbe(30), Alvin Mbingi (30) Charles Kachoma(20), Fabian Mwananyali (18) na dereva bodaboda, Alex Tung’ombe(27).
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Erick Kamala akisaidizana na Aaron Titus mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya wakati washtakiwa hao walipofikishwa mahakamani hapo.
Akiwasomea mashtaka yao Wakili Kamala alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 50 likiwemo moja la kuongoza genge la uhalifu, kumi na mbili ya kutuma jumbe zenye ushawishi, 17 ya kutumia line ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, 19 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na moja ni mashtaka ya utakatishaji fedha.
Katika mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu wakili Kamala alidai kati ya Septemba Mosi, 2023 na Mei 5, mwaka huu katika maeneo yasiyojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania washtakiwa wote kwa pamoja waliongoza genge la uhalifu na kujipatia kiasi cha Sh milioni 9,2000,000
Miongoni mwa jumbe hizo za ushawishi zilikuwa zikisema “666 jiunge na chama huru cha free mason Tanzania umiliki mali pesa majumba mvuto vipaji pete bila kafala kwa kujiunga.” na “mzee tadeo mgaga anatibu kisukari uzazi kifafa dawa ya pesa mapenzi guvu za kiume kurudisha mme au mke makesi kuvuta wateja zidiko nyota tiba mbalimbali mpigie na 0682280646.”
Mashtaka mengine inadaiwa washtakiwa wote 12, kati ya Septemba mosi, 2023 hadi Mei 5, mwaka huu washtakiwa wakiwa katika katika maeneo yasiyojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitakatisha fedha kiasi cha 9,200,000 zao la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote.
Wakili Titus alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.
Hakimu Mbuya alisema kosa la utakatishaji fedha halina dhamana hivyo washtakiwa wote walirudishwa rumande.
Kesi iliahirishwa hadi Juni 27, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.